Saturday 12 March 2016

JELA KWA KUMKATA SEHEMU ZA SIRI MKEWE


MKAZI wa kata ya Mbugani mjini Tabora, Mashaka Maziku (60) amehukumiwa kwenda jela miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kumkata mkewe sehemu za siri kwa imani za kishirikina ili ajipatie mali.

Aidha, Maziku na mshirika wake ambaye ni mganga wa kienyeji, Kahele Paul, wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kula njama ya kutenda kosa. Walihukumiwa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Jackton Rushwela baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.

Hakimu Rushwela alisema anamhukumu Maziku kwenda jela miaka saba, iwe fundisho kwa wananchi wengine wanaokuwa na tamaa ya kujipatia mali kwa njia za kishirikina huku wakiwasababishia madhara watu wengine.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na Wakili wa Serikali, Idd Mgeni, washtakiwa walitenda makosa hayo mwaka juzi, kati ya Oktoba 29 na Novemba 2 katika eneo la Kazaroho kata ya Mbugani mjini Tabora.

Ilidaiwa kwamba Maziku aliambiwa na mganga wa kienyeji ambaye ni mshtakiwa wa pili , kwamba akipeleka sehemu za siri za mkewe atapata Sh milioni tano. Mahakama ilielezwa kwamba, Maziku baada ya ushauri huo huku akiwa na tamaa ya kujipatia mali, alimchukua mkewe (jina tunalihifadhi) na kwenda kumnywesha pombe kabla ya kutimiza ukatili huo.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne ambao waliiambia Mahakama kwamba mshtakiwa baada ya kumnywesha pombe nyingi mkewe alichukua kisu na kumkata sehemu za siri na kuzihifadhi kwenye mfuko wa suruali yake na akatoweka.

Walibainisha kuwa mama huyo alikuwa akipiga kelele kutokana na maumivu makali aliyopata huku akivuja damu nyingi na aliokolewa na majirani na kumpeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu.

Maziku baada ya kukamatwa na kuhojiwa, alikana akidai kwamba yeye aliondoka na kumwacha mkewe akiwa ni mzima, lakini ulipofanyika upekuzi, nyama ya nyeti hizo zilikutwa kwenye mfuko wa suruali yake.

Upande wa mashitaka uliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa, kwani vitendo vya ukatili vya aina hiyo kwa ajili ya kujipatia mali, vimekuwa vinawasababishia madhara watu wasiokuwa na hatia.

No comments:

Post a Comment