Wednesday 8 June 2016

MAANA YA FUNGA(SAUMU) NA BARAKA ZAKE


Maana ya funga (Saum)
MAANA ya kufunga (saum) ni kujizuilia. Neno Saumu kwa maana ya kujizuilia linaweza kutumika katika kujizuia kufanya jambo lolote la kawaida mtu alilozoea kulifanya. Katika Qur'an tunafahamishwa kuwa Bibi Maryam baada ya kumzaa Nabii Issa (a.s.) alijizuia (alifunga) ili asiseme na mtu neno lolote juu ya mtoto wake.
"...Na kama ukimwona mtu yoyote (akauliza habari za mtoto huyu) sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rehema ya kufunga, kwa hiyo leo sitasema na mtu". (19:26).
Katika Uislamu kufunga (saumu) ni kujizuilia kula, kunywa, kuvuta sigara, kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na masikio, kujizuia na kujamii, kujitoa manii kwa makusudi au kwa matamanio na kujizuia kujitapisha kwa ajili ya Allah (s.w.), kwa kipindi cha kati ya Al-fajri ya kweli mpaka kuingia magharibi. Hii ndio maana ya nje ya Saumu katika Uislamu.
Kufunga katika Uislamu kuna maana ya ndani zaidi, ambayo kama haikufikiwa, kuzuilia kufanya vitendo hivyo vilivyoelezwa hakutakuwa na maana yoyote kwa mfungaji.
Kufunga kwa maana ya ndani ni pamoja kujizuilia kutenda maovu yote yaliyokatazwa na Allah (s.w). Ili saumu ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono na miguu- pamoja na fikra na hisia zake na matendo aliyokataza Allah (s.w.).
Funga ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Allah (s.w.); Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza Allah (s.w.) kama vile kusengenya, kusema uwongo, kugombana na kadhalika, funga ya masikio ni kujizuia kufanya yale yote aliyoyaharamisha Allah (s.w.); funga ya miguu ni kujizuilia na kuendea yale yote aliyoyakataza Allah (s.w.) funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allah (s.w.). Ni katika maana hii Mtume (s.a.w.) anasema katika Hadithi zifuatazo:
Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Yule ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yaani Allah (s.w.) hana haja na funga yake. (Bukhari).
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Ni wangapi wanaofunga lakini hawana funga ila kukaa na kiu tu ni wangapi wanao swali usiku ambao hawana swala ila huambulia kupoteza usingizi tu. (Darimi).
Hadithi hizi zinatuthibitishia kuwa ufungaji usioambatana na kujizuia na mambo maovu na machafu, haumpatii mfungaji faida yoyote.
Umuhimu wa funga katika Uislamu
Funga ya Ramadhani ni miongoni mwa nguzo za Uislamu na ni faradhi kwa Waislamu kama inavyobainika katika aya ifuatayo:
Enyi mlioamini! Mmeamrishwa kufunga (saumu) kama walivyofaradhishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu. (2:183)
Kama ilivyo katika nguzo nyingine za Uislamu, mtu atakapoivunja makusudi nguzo hii hatabakia kuwa Muislamu japo atajiita Muislamu na watu wakaendelea kumwita hivyo. Katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas, Mtume (s.a.w.) amesema:
Kuna viungo vitatu vinavyomuunganisha Muislamu na dini ya Uislamu na yeyote yule atakayevunja kiungo kimoja katika hivi atakuwa amekana Uislamu na kuuawa kwani ni halali. Viungo hivi ni: Kushuhudia kuwa hapana Mola ila Allah, Kusimamisha Swala tano na kufunga mwezi wa Ramadhani.
Katika Hadithi nyingine Abu-Hurairah (r.a.) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w.) amesema:
Yeyote yule atakaye acha makusudi kufunga siku moja ya mwezi wa Ramadhani, hawezi kuifidia siku hiyo hata akifunga kila siku katika umri wake wote (uliobakia). (Abu-Daud)
Funga ni ibada maalum iliyo muhimu sana katika kumuandaa mja kuwa mcha Mungu kwa kule kukataa kwake matamanio ya kimwili. Hivyo Allah (s.w.) kwa ukaribu wake ameahidi malipo makubwa kwa wenye kutekeleza ibada hii ili iwe motisha kwao ya kuwawezesha kutekeleza ibada hii kwa hima kubwa na kwa ukamilifu unaotakikana kama tunavyojifunza katika Hadithi zifuatazo:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Mwenye kufunga Ramadhani akiwa na imani na akawa na matumaini ya kupata malipo kutoka kwa Allah dhambi zake zote zilizopita husamehewa, Na mwenye kusimama kwa swala (tarawehe) katika mwezi wa Ramadhani akiwa na imani na matumaini ya kupata malipo (kutoka kwa Allah), dhambi zake zote zilizopita zitasamehewa. Na yule atakayesimama (kwa swala) katika usiku uliobarikiwa (Lailatul-Qadri) akiwa na imani na matumaini ya kupata malipo kutoka kwa Allah (s.w.) dhambi zake zote zilizotangulia zitasamehewa. (Bukhari na Muslim).
Pia Abu-Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: Kila amali njema anayoifanya mwanaadamu italipwa mara kumi (Al-Qur'an 6:160) mpaka kufikia mara mia saba (Al-Qur'an 2:261). Allah (s.w.) amesema:
Ila kufunga kwa sababu funga ni kwa ajili Yangu, na ni mimi mwenyewe nitakayeilipa. Mwenye kufunga anakata matamanio yake ya kimwili na anaacha chakula kwa ajili yangu. Kwa mwenye kufunga kuna furaha mbili, furaha moja anaipata wakati wa kufuturu na nyingine wakati atakapokutana na Mola wake. Na hakika harufu ya mdomo wa mwenye kufunga ni bora mbele ya Allah (s.w.) kuliko harufu ya miski. Na funga ni ngao. Kwa hiyo atakayefunga miongoni mwenu hataongea maneno ya upuuzi wala hatagombana. Kama itatokea achokozwe na yeyote, au mtu atakakupigana naye, na aseme: Nimefunga. (Bukhari na Muslim).
Vile vile Mtume (s.a.w.) katika kusisitiza umuhimu wa funga ya Ramadhani alitoa khutuba mwishoni mwa mwezi wa Shaaban kama ilivyonukuliwa katika hadithi ifuatayo:
Salman al-Farisy ameeleza: Mtume (s.a.w.) alituwaidh mwisho mwa siku ya Shaabani akasema: Enyi watu! Hakika umekujieni mwezi mtukufu, mwezi uliobarikiwa, mwezi ambao ndani yake kuna usiku uliobora zaidi kuliko miezi elfu moja. Allah (s.w.) amefaradhisha kufunga katika mwezi huu na kusimama (kwa swala ya tarawehe) katika mausiku yake ni sunnah. Atakayetekeleza kitendo kizuri kisicho faradhi atapata ujira wa mtu aliyetekeleza kitendo cha faradhi katika miezi mingine, na yule atakayetekeleza kitendo cha faradhi atapata ujira wa mara 70 wa ujira wa kitendo hicho katika miezi mingine. Na ni mwezi wa subira, na ilivyo, subira malipo yake ni pepo. Na ni mwezi wa kuhurumiana na mwezi ambao mahitaji (mapato) ya muumini huongezwa. Atakayetoa futari kwa mwenye kufunga katika mwezi huu kuna kusamehewa dhambi zake na kuwekwa huru na moto, na atapata malipo sawa na ya yule aliyefunga bila ya yeye kupunguziwa chochote. Tukauliza: Ee Mtume wa Allah! Hakuna yeyote kati yetu mwenye uwezo wa kumfuturisha mtu aliyefunga. Alijibu Mtume: Allah atamlipa yule mwenye kumfuturisha aliyefunga kwa funda la maziwa, au tende moja au funda la maji. Na yule anayekidhi haja ya mtu Allah atamnywesha kutokana na Birika (Kawthar) langu na hatakuwa na kiu mpaka atakapoingia peponi.
Na (Ramadhani) ni mwezi ambao mwanzo wake kuna kurehemewa, katikati yake kuna kusamehewa na mwisho wake kuna kuachwa huru na moto. Na yule atakayempunguzia kazi mtumwa (mfungwa vita) wake, Allah atamsamehe, na atamuacha huru na moto.
Historia ya kufunga
Funga, kama ilivyo katika ibada nyingine kama tulivyoona katika kusimamisha swala na kutoa zakat, imetekelezwa na Mitume wote pamoja na umma zao. Allah (s.w.) ametukumbusha hili wakati alipotupa amri ya kutekeleza ibada hii maalum, kama tunavyorejea katika Qur'an:
Enyi mlioamini! Mmeandikiwa (mmefaradhishiwa) kufunga kama walivyofaridhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu. (2:183)
Katika historia tunajifunza kuwa, kila Mtume alipoondoka, baada ya kipindi kupita, watu waliacha mafundisho yake na kuingia katika ushirikina. Lakini bado tunakuta funga, japo si katika madhumuni na asili yake iliyoachwa na Mitume wa Allah (s.w.), imebakia katika jamii za kishirikina kwa kipindi chote cha historia. Hebu tuangalie mifano michache ya dini za ushirikina ambapo funga, kwa maana ya kushinda na njaa na kiu, imekuwa miongoni mwa ibada muhimu za dini hizo.
Jamii ya Nabii Ibrahim
Nabii Ibrahim (a.s.) aliinuliwa katika jamii ya washirikina. Walikuwa wakiabudu jua, mwezi, nyota na masanamu chungu nzima waliyoyachonga wenyewe. Pamoja na ushirikina wao huo walikuwa wakifunga siku 30 mfululizo katika kila mwaka kwa heshima ya mwezi
Wahindu (Hinduism)
Dini ya Kihindu ni miongoni mwa dini za kishirikina katika bara la India. Katika dini hii funga, ni kitendo kilichosisitizwa sana japo si lazima, katika siku maalum kama vile kupatwa kwa jua, kumbumbuku ya kuzaliwa mwanzilishi wa dini yao na kadhalika. Funga kwao ni kujizulia na kula na kunywa kuanzia alfajiri mpaka saa tisa mchana.
Mayahudi (Judaism)
Dini ya Kiyahudi ni dini waliyoibuni Mayahudi baada ya Nabii Musa (a.s.) ambapo walimfanya Uzairi mwana wa Mungu. Pamoja na hivyo wachaji wa Kiyahudi walikuwa wakifunga Alhamisi na Jumatatu kama kumbukumbu ya kwenda na kurudi kwa Nabii Musa (a.s.) katika safari yake ya Sinai kwenda kuchukua Taurati. Kutokana na kumbukumbu ya historia, Nabii Musa alikwenda kwenye mlima Sinai siku ya Alhamisi na kurejea siku ya Jumatatu baada ya siku arobaini kupita.
Pia Mayahudi hufunga kwa saa 24 katika kila mwezi 10 Muharamu, kwa kumbukumbu ya siku Wanaisraili ( Mayahudi) walipookolewa na Allah (s.w) kutokana na udhalimu wa Firaun. Siku hii ambayo hata Waislamu wamesuniwa kufunga huitwa siku ya Ashuurah.
Pamoja na funga hizi, pia Mayahudi wana tabia ya kufunga mara kwa mara kulingana na haja. Kwa mfano mtu anaweza kuamua kufunga siku kadhaa kama kumbukumbu ya matukio fulani katika maisha yake, au anaweza kufunga funga kama kitubio cha madhambi yake, au anaweza kufunga wakati akiwa na matatizo ili kupata huruma ya Mungu.
Ukiacha siku ya Ashuura ambapo funga huchukua saa 24, funga za Mayahudi huanza alfajiri na huishia pale inapojitokeza nyota ya kwanza usiku.
Wakristo
Dini ya Ukristo imebuniwa baada ya Nabii Issa (a.s.). Katika dini hii Nabii Issa (a.s.) amefanywa mwana wa Allah (s.w.) na kwamba yeye ndiye mkombozi wa Wakristo. Pamoja na hivyo, Wakristo wanakiri kuwa kufunga ni kitendo cha uchaji - katika dini yao. Wakristo wa mwanzo walikuwa wakifunga siku 40 mfululizo kasoro siku za Jumapili kama kumbukumbu ya siku zile alizofunga Yesu (Nabii Issa a.s.) kama inavyobainishwa katika Biblia.
Historia inatuonyesha vile vile kuwa funga hizi za Washirikina zimetofautiana sana katika mfumo na funga ya Kiislamu aliyoiamrisha Allah (s.w.). Ambapo Waislamu wakifunga hujizuia kula, kunywa na kujamii mchana kutwa kuanzia alfajiri mpaka kuchwa kwa jua, funga za washirikina zilichukua mifumo mbalimbali. Wengine walijizuilia kula na kunywa tu lakini waliendelea kujamii, wengine walijizulia kunywa na kula kuanzia alfajiri mpaka saa 9 alasiri, wengine walijizulia kula aina fulani tu ya chakula kama vile nyama, wengine walijizulia kwa kunywa tu maji yaliyochanganywa na chumvi au maji ya ndimu, na kadhalika.

No comments:

Post a Comment